Kiswahili 01. Taurati na Injili… uongozi kwa watu!

Assalamu’alaikum!
Kurani Tukufu yatuambia kwa nini sisi twahitaji kusoma Taurati na Injili (ya Maandiko ya Biblia). Katika Sura 3:3 yatuambia haya yafuatayo:

 

‘Amekuteremshia (hatua kwa hatua) Kitabu kwa haki, kinachosadikisha yaliyokuwa kabla yake. Na aliteremsha Taurati (Sheria ya Musa) na Injili (ya Yesu) zamani – ziwe uongozi kwa watu, Na akateremsha vitabu vingine vya kupambanua (baina ya haki na batili).’
Inaeleza wazi kabisa ya kwamba Taurati (Sheria) na Injili vilitolewa kwa ajili ya watu wote… “ziwe uongozi kwa watu”. Watu hujumuisha watu wote, siyo tu wachache walioteuliwa.

Twafundishwa katika Kurani Tukufu Sana kwamba kwa njia ya Isa al-Masih (Kristo Masihi) hiyo Injili iliteremshwa. Iliteremshwa kuwa ‘uongozi’ na kuwa ‘mauidha’ kwa wamchao (Mwenyezi Mungu). Sura 5:46

‘Na tukawafuatishia (Mitume hao) Isa bin Maryamu kuyahakikisha yaliyokuwa kabla yake katika Taurati (Sheria), na tukampa Injili iliyomo ndani yake uongozi na nuru na isadikishayo yaliyokuwa kabla yake katika Taurati, na uongozi na mauidha kwa wamchao (Mwenyezi Mungu).’ 005:046 Al Maidah.
Mauidha haya (Taurati na Injili) ni onyo, au karipio dhidi ya makosa, yanatushauri tusijiingize katika matendo mabaya. Mauidha haya ni ya kutufundisha sisi na kutuongoza tukiwa bado tumo humu katika Sayari Dunia. Watu wenye akili timamu, ambao sikio lao liko tayari kupokea mafundisho ya Mwenyezi Mungu, daima watatii maonyo yatokayo Mbinguni, kama vile alivyofanya Musa katika (Injili) Waebrania 8:5. Mwenyezi Mungu ameyalinda kwa makini Maneno yake kama ilivyoandikwa katika Sura 5:48. “Na tumekuteremshia Kitabu kwa (ajili ya kubainisha) haki, kinachosadikisha vitabu vilivyokuwa kabla yake, na kuvihukumia …. Ni faraja iliyoje kujua kwamba Mwenyezi Mungu anayalinda Maneno yake na kuyahukumia, ili sisi leo tupate kuwa na uongozi hakika kuhusu yale yaliyo ya haki na yaliyo batili.

Je! Taurati na Injili vimechafuliwa?
Lisingekuwa jambo la kushangaza kwetu kuona mambo mengi ya kujenga yameandikwa juu ya Vitabu hivi Vitakatifu (Taurati na Injili) katika Kurani Tukufu Sana! Hata hivyo, licha ya hayo yote, watu wenye makusudi mazuri watakuambia kwamba vitabu hivi vimechafuliwa! Fikiria kusema mambo kama hayo juu ya Vitabu hivi Vitakatifu vilivyoteremshwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu? Ni kufuru kwake! Kana kwamba Mungu Mwenyezi hawezi kuyalinda maneno yake mbali na watu wenye mawazo mabaya! Lakini kutoka kwa watu hao hao wasemao kwamba Vitabu hivi Vitakatifu vya Taurati na Injili vimebadilishwa au kuchafuliwa utaona wananukuu kwa wingi kutoka katika vitabu hivyo kuendeleza fikara zao! Hata wanakariri sehemu kubwa za Maandiko ya Biblia na halafu wanasema yamechafuliwa, tena watakuambia kuwa haya si Maneno yake Mwenyezi Mungu! Enyi rafiki kama hivyo ndivyo mambo yalivyo, kwa nini myajaze mawazo yenu na vitabu ambavyo vimechafuliwa? Nyakati zingine wananukuu kwa wingi kutoka katika vitabu hivi vinavyodhaniwa vimechafuliwa ili kuthibitisha wazo lao, lakini wanawezaje kuwa na hakika kwamba kile wanachonukuu hakijachafuliwa? Enyi rafiki, haya yote yangetuambia sisi kwamba mawazo ya watu hao yameshawishiwa sana na Ibilisi (Shetani). Mungu Mwenyezi ajua fika alifanyalo! Hebu na tumwamini na kutulia juu ya Maneno yaliyoteremshwa kutoka kwake na kuyatwaa maneno haya na kuyafanya yawe yetu wenyewe. Rudia tena kusoma maneno ya Sura 5:46 yasemayo kwamba Injili iliteremshwa kwa njia ya Isa al-Masih iwe uongozi na mauidha kwa wale wamchao Mungu Mwenyezi. Mpendwa wangu msomaji, je, unamcha Mwenyezi Mungu? Basi maneno haya yameandikwa kwa ajili yako wewe!

Mawe ya Umbali…
Siku hizi watu wanahitaji kuelekezwa. Mara ngapi watu wanaosafiri katika njia kuu nyingi wanaangalia Mawe ya umbali barabarani kujua njia ipi na umbali gani kwenda kwenye mji walioukusudia. Katika ulimwengu huu, sisi sote tunahitaji mawe ya umbali kutuambia njia ipi tusafiri salama ili tuweze kufika Mbinguni tuendako. Vitabu hivi Vitakatifu (Maandiko) ni mawe ya umbali (miongozo) ambayo yatakusaidia, na kukufanya usipotee njiani. Kwa maana hakika hakuna anayefurahia kwenda njia isiyo yenyewe, hilo ni jambo la kuvunja moyo sana kusema kwa machache. Lakini leo hii watu wengi mno wanasafiri katika maisha na hata hawatambui kwamba wamo katika barabara kuu iliyokosewa.
Kurani Tukufu yatuambia ‘mwaminini Mwenyezi Mungu na Mtume wake … na Vitabu alivyoviteremsha zamani.’ Sura 4:136. Kwa maana wale wote wanaowakanusha “Mitume wake… Vitabu vyake” wamepotea na kwenda mbali sana.
Watu wameukataa uongozi na nuru, iliyoteremshwa, na wamechagua badala yake kubaki katika giza la ulimwengu huu. Ibilisi (Shetani) amepofusha macho yao kweli, lakini Mwenyezi Mungu kwa Rehema, anatuita tuje kwenye nuru tukufu ya ile kweli kama ipatikanavyo katika Maandiko (Biblia).

Kurani Tukufu Sana yasema kwamba “Huu ni ukweli uliotoka kwa Mola wenu” Sura 18:29. Umuhimu wa ule ukweli hauwezi kusisitizwa kupita kiasi. Ni kwa njia ya ule ukweli Mwenyezi Mungu anawatakasa watu wake. Imeandikwa hivi katika Injili, Yohana 17:17 – “Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli.” Neno lake Mwenyezi Mungu ndiyo kweli.
Kwa hakika kabisa, Mwenyezi Mungu ni mwenye hekima tosha na mwenye uwezo tosha kuweza kuhukumia na kuyalinda Maneno yake. Hii hutukumbusha tena katika Sura 6:115 – “Na yametimia maneno ya Mola wako kwa kweli na uadilifu. Hakuna awezaye kuyabadilisha maneno Yake. Na Yeye ndiye asikiaye (na) ajuaye.” Mungu anapendezwa kutupa sisi kweli yake.
Imenenwa ya kwamba katika “Injili iliyomo ndani yake [umo] uongozi na nuru na isadikishayo yaliyokuwa kabla yake katika Taurati”. Sura 5:46
Kwa hakika hata Mtume Muhammad aliyewatia moyo Waislamu kusoma Injili alijua yale yaliyokuwamo ndani ya hiyo Injili, kwa maana angewezaje kusema kwamba ilikuwa uongozi na nuru kama yeye alikuwa hajui yale yaliyokuwa yameandikwa mle.
Endapo Mtume Muhammad asingetaka sisi tuisome Injili au Taurati, basi, asingekuwa amesema maneno yenye nguvu kama hayo kusadikisha kwamba Injili na Taurati ni uongozi kwetu leo. Kwa maana yeye alisema viwe uongozi kwa “wale wamchao Mwenyezi Mungu”. Sura 5:46. Rafiki zangu, mkimcha Mwenyezi Mungu, basi, ninyi pia mtatumia muda wenu fulani kuyasoma Maandiko ya Biblia. Kwa maana ni kweli kwamba yanatoa uongozi kwa watu.
Ni katika Maandiko ya Biblia, kama Kurani Tukufu isemavyo, twaweza “Kupambanua” baina ya haki na batili (Sura 3:3-4). Kamusi yatuambia kwamba “Kupambanua” (Criterion) ni ‘kanuni’ ambayo mambo yote yapaswa kupimwa kwayo kama ni ya haki au batili. Wote watahukumiwa kwa kanuni hii, kwa maana Nabii Isaya (Taurati) alisema katika sura ya 8:20 – “Na waende kwa Sheria (Taurati) na Ushuhuda; ikiwa hawasemi sawasawa na neno hili, bila shaka kwa hao hapana asubuhi.” Kwa Sheria, hii inahusu ile Sheria ya Amri Kumi, na kwa Ushuhuda, ni ushuhuda wa Maandiko, kama maneno ya mtu awaye yote hayaafikiani na yale yaliyoandikwa, basi, hapo hakuna nuru ndani yao. Katika Injili, Isa al-Masih anatufunulia sisi jinsi itupasavyo kuishi. ‘Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu [Allah].” Mathayo 4:4
Je, kuna ajabu yo yote, basi, ya kwamba Mstahiki Nabii Muhammad alitoa mauidha yake mengi sana kwetu yanayotuelekeza sisi kwenye Maandiko ya Biblia?

Taa na Mwanga…

Katika Kurani Tukufu, Sura 17:55, inasema kwamba mitume wengine walipewa vipawa, na kwa Daudi alipewa kipawa cha Zaburi. Katika Zaburi inasema hivi kuhusu Neno la Mwenyezi Mungu, “Neno lako ni taa ya miguu yangu, na Mwanga wa njia yangu” Zaburi 119:105. Hivi umejaribu kutembea katika giza la usiku bila mwanga? Je, uliona vigumu kabisa kutembea pasipo kuwa na hofu ya kuanguka chini au kukanyaga mahali fulani ambapo ungejeruhiwa au hata vibaya zaidi kuanguka chini ya genge refu?
Dunia yetu imo katika giza la usiku, kama ulikuwako wakati tulipohitaji taa kwa ajili ya miguu yetu, ni leo. Watu wengi sana wamepotea mbali sana kutoka kwenye njia ya haki, wameitupilia mbali “Taa” na “Mwanga” ambao kwa huo twaweza kuijua njia sahihi. Kwa nini siku hizi kuna uhalifu mwingi sana, uasi, mmomonyoko wa maadili? Kwa nini jamii iko ukingoni mwa maangamizi? Je, hawajamkana Mungu Mwenyezi, Sheria [Taurati] yake, Vitabu Vyake na mitume wake? Sura 4:136. Hivyo, basi, kila mmoja anasisitiziwa, haidhuru wewe uwe nani, kusoma “Maandiko ya Biblia” ambayo kwa rehema yameteremshwa kwetu kutoka Mbinguni. Hayo kwa hakika yamekuwa ndiyo “kanuni” kwa ajili yetu. Kutufundisha sisi yaliyo ya haki na yaliyo haramu.
Kabla hujafungua kurasa zake, daima mwombe Mungu Mwenyezi akufundishe ili upate ufahamu sahihi unaposoma. Mungu Mwenyezi huwabariki wale ambao kwa unyofu wa moyo wanajifunza na kuitafuta haki. (Taurati) Yeremia 29:13 – ‘Nanyi mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote.’ Wale wamtafutao Mungu Mwenyezi yawapasa kumtafuta kwa moyo wao wote. Mungu Mwenyezi na awabariki sana.

Maandiko haya yamenukuliwa kutoka DivineIslam’s Qur’an Viewer software V2.913

Mafungu ya Biblia yametoka katika Toleo la King James (KJV).

“BISMILA-HIR RAHMA-NIR RAHIM”.

Kwa kujifunza zaidi: www.salahallah.com

‘Taurati
Na
Injili
… uongozi kwa watu!

Sura 3:3-4
Aali Imran

Mfululizo Na. 01