BISMILA-HIR RAHMA-NIR RAHIM

Asalamu Aleikum!
Mpendwa msomaji, hebu leo hii na iwe juu yako Amani na Huruma itokayo kwa Mwenyezi Mungu, ambaye ni mwingi wa kusamehe na mwingi wa kurehemu! (Sura 2:226 Al Baqarah). Hii ni Sehemu ya Pili ihusuyo somo la Hukumu. .
Katika vyote viwili, yaani, Kurani Tukufu na Vitabu Vitakatifu, somo hili la Saa ya Hukumu mara nyingi linaongelewa juu yake. Kwa kweli, hiyo imetajwa mara 77 katika Kurani Tukufu kama “Siku ya Hukumu” au “Siku ya Kiama” Katika Vitabu Vitakatifu vya Maandiko, tukio hilo mara nyingi linatajwa kama “Siku ya Bwana.” Katika siku hiyo wenye dhambi wote, isipokuwa kama kabla yake walikuwa “wakitubu na kudumu kuamini na kufanya yaliyo mema” (Sura 19:60 Maryam), watapokea ujira wao…”, yaani, “adhabu ya Moto mkali.” Sura 22:4 Al-Hajj.
Maonyo hutangulia Adhabu
Mwenyezi Mungu katika upendo wake na rehema zake ametuambia mapema kabla ya wakati ule, jinsi ya kutoka na kuwa hai na safi katika Hukumu hiyo. Siku zote kabla Mungu hajatuma hukumu zake juu ya mataifa, miji mikubwa au wanadamu, anatuma onyo kuonesha jinsi wawezavyo kuikwepa hukumu hiyo. Watu wakigeuka na kuziacha njia zao mbaya, hukumu inaweza kuahirishwa kwa muda fulani. Lakini kama watu hao wakiendelea tu kuzivunja Sheria Takatifu za Mungu, hukumu hiyo hatimaye huwaangukia. Tunaikuta mifano yake wakati Mwenyezi Mungu alipomtuma Yona (Yunus) kwenda kwenye mji mkubwa wa kale uliojaa maovu wa Ninawi, “Basi neno la BWANA lilimjia Yona, mwana wa Amitai, kusema, Ondoka, uende Ninawi, mji ule mkubwa, ukapige kelele juu yake; kwa maana uovu wao umepanda juu mbele zangu.”
Mwenyezi Mungu pia alimtuma Nuhu kipindi kirefu kabla ya wakati huo kuwaonya wakazi wa dunia juu ya gharika iliyokuwa ikija. Nuhu aliagizwa kujenga safina ili kuikwepa ile gharika. Mwanzo 6 na 7.
Swali lake Mwenyezi Mungu!
“Mbona mnataka kufa, wewe na watu wako, kwa upanga, na kwa njaa, na kwa tauni, kama BWANA alivyosema…” Yeremia 27:13
“Tupilieni mbali nanyi makosa yenu yote mliyoyakosa; jifanyieni moyo mpya na roho mpya; mbona mnataka kufa…” Ezekieli 18:31
Haya ndiyo matokeo yatakayotokea twendapo kwa Mungu na kumwomba atupe moyo mpya na roho mpya…
“Ndipo mtazikumbuka njia zenu mbaya, na matendo yenu yasiyokuwa mema, nanyi mtajichukia nafsi zenu kwa macho yenu, kwa sababu ya maovu yenu na machukizo yenu.” Ezekieli 36:31.
Mtaichukia njia yenu ya kwanza ya maisha maovu na mawazo machafu! Mwenyezi Mungu ni wa kushangaza, kama sisi tutamruhusu afanye kazi yake kwa uhuru katika maisha yetu. Hii yote ni sehemu ya utakaso unaoendelea wakati Masihi Isa bado yumo ndani ya Patakatifu pa Mbinguni kule juu. Utakaso wa mioyo yetu na maisha yetu ya dhambi pamoja na matokeo yake yateketezayo.
Hebu na uziangalie ahadi hizi nzito zitokazo kwa Mwenyezi Mungu! Hapo kale Mwenyezi Mungu aliwaambia watu wake…
“Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, sikufurahii kufa kwake mtu mwovu; bali aghairi mtu mwovu, na kuiacha njia yake mbaya, akaishi. Ghairini, ghairini, mkaache njia zenu mbaya, mbona mnataka kufa…?” Ezekieli 33:11
Kuhukumiwa Mbele zake Mwenyezi Mungu
Kuna wakati ambapo dunia yote na wakazi wake wote itawapasa kuhukumiwa mbele zake Mungu. Pale itaonekana iwapo wanastahiki kupokea Uzima wa Milele. Tangazo hilo la hukumu kama hiyo limeandikwa katika kitabu kile cha mwisho cha Ufunuo.
“Kisha nikaona malaika mwingine, akiruka katikati ya mbingu, mwenye Injili ya milele, awahubiri hao wakaao juu ya nchi, na kila taifa na kabila na lugha na jamaa, akasema kwa sauti kuu, Mcheni Mungu, na kumtukuza, kwa maana saa ya hukumu yake imekuja. Msujudieni yeye aliyezifanya mbingu na nchi na bahari na chemchemi za maji.” Ufunuo 14:6-7
Kutoka katika Kisiwa cha upweke cha Patmo, Yohana au Yahaya, mwandishi wa Ufunuo anaandika kwa wazi:
“Kisha nikaona kiti cha enzi, kikubwa, cheupe, na yeye aketiye juu yake;… Nikawaona wafu, wakubwa kwa wadogo, wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi; na vitabu vikafunguliwa; na Kitabu kingine kikafunguliwa, ambacho ni cha Uzima; na hao wafu wakahukumiwa katika mambo hayo yaliyoandikwa katika vile vitabu, sawasawa na matendo yao. Bahari ikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake. Wakahukumiwa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake.” Injili Ufunuo 20:11-13
Hakuna atakayeikwepa hukumu hiyo
”Kwa maana imetupasa sisi sote kudhihirishwa mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mtu apokee ijara ya mambo aliyotenda kwa mwili, kadiri alivyotenda, kwamba ni mema au mabaya.”
2 Wakorintho 5:10
“Kwa maana Mungu ataleta hukumuni kila kazi, pamoja na kila neno la siri, likiwa jema au likiwa baya.” Mhubiri 12:14
Mpango wa Mwenyezi Mungu wa Kukutakasa wewe na Kukuokoa
“Yeye aliye na Mwana, anao huo Uzima; asiye naye Mwana wa Mungu hana huo uzima.” 1 Yohana 5:12
Mpango wa Mwenyezi Mungu ni kukuthibitisha wewe katika Hukumu hiyo. Yupo pale kukushika mkono wako. Hebu na uiangalie aya hii kutoka Isaya. “Haya, njoni, tusemezane, asema BWANA. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu.” Taurati Isaya 1:18
”Maana yale yasiyowezekana kwa sheria, kwa vile ilivyokuwa dhaifu kwa sababu ya mwili, Mungu, kwa kumtuma Mwanawe mwenyewe katika mfano wa mwili ulio wa dhambi, na kwa sababu ya dhambi, aliihukumu dhambi katika mwili.” Injili Warumi 8:3
Sasa ni wasaa wetu wa kuziungama dhambi zetu na kuzipeleka mapema hukumuni: “Dhambi za watu wengine zi dhahiri, zatangulia kwenda hukumuni; wengine dhambi zao zawafuata.” 1 Timotheo 5:24
Leo ndio wakati wa kumpokea Masihi Isa kama sadaka yako ya dhambi. Isa anaweza kukuokoa kabisa katika hukumu ile ya mwisho, lakini iwapo tu sisi tumempokea yeye kama Mwokozi wetu binafsi. Shauku ya Mungu ni kuwaokoa wote.
“Ambaye hutaka watu wote waokolewe, na kupata kujua yaliyo kweli. Kwa sababu Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, Mwanadamu Kristo Yesu; ambaye alijitoa mwenyewe kuwa ukombozi kwa ajili ya wote, utakaoshuhudiwa kwa majira yake.” 1 Timothewo 2:4-6
Hapa ni picha ya kile atakachofanya Mungu kwa wale wanaompenda! Enyi rafiki zake Mwenyezi Mungu, je! mwampenda?
“Maana nitawatwaa kati ya mataifa, nami nitawakusanya na kuwatoa katika nchi zote, na kuwarudisha katika nchi yenu wenyewe. Nami nitawanyunyizia maji safi, nanyi mtakuwa safi, nitawatakaseni na uchafu wenu wote, na vinyago vyenu vyote. Nami nitawapa ninyi moyo mpya, nami nitatia roho mpya ndani yenu, nami nitatoa moyo wa jiwe uliomo ndani ya mwili wenu, nami nitawapa moyo wa nyama. Nami nitatia Roho yangu ndani yenu, na kuwaendesha katika sheria zangu, nanyi mtazishika hukumu zangu, na kuzitenda. Nanyi mtakaa katika nchi ile niliyowapa baba zenu, nanyi mtakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wenu. Nami nitawaokoeni na uchafu wenu wote, nitaiita ngano, na kuiongeza, wala sitaweka njaa juu yenu tena.” Ezekieli 36:24-29
Rafiki zangu, je, mnao uchafu? Je, mnayo mambo fulani katika maisha yenu yanayohitaji kutakaswa? Hivi ndivyo anavyojaribu kufanya Mwenyezi Mungu kwa kila mmoja wetu wakati Isa angali bado ndani ya Patakatifu pa Mbinguni. Je, tutamruhusu afanye kazi yake ya kimbingu? Je, tutasema kwake ndiyo daima?
Mwombezi wa Mwanadamu ni Isa
Kwa hiyo ni mpango wa Mwenyezi Mungu kuokoa, je, utafanya kazi pamoja naye ili akuokoe? Je, utamruhusu akuokoe kwa njia yake aliyoichagua yeye?
“Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.” Matendo 4:12
Jina hilo linalostahiki si jingine ila ni lake Masihi Isa, Mwokozi wa wanadamu wote. Je, utampokea katika maisha yako?
Zamani sana ilitabiriwa na Mwenyezi Mungu kupitia manabii wale wa kale, ya kwamba Mwenyezi Mungu angemteremsha Mmoja ambaye angeweza kumhesabia haki mwenye dhambi.
“Ataona mazao ya taabu ya nafsi yake, na kuridhika. Kwa maarifa yake mtumishi wangu mwenye haki atawafanya wengi kuwa wenye haki; Naye atayachukua maovu yao.” Isaya 53:11
Siku ya Upatanisho
Hapo kale hiyo iliitwa Siku Kuu ya Upatanisho. Siku hiyo Israeli wote walitakiwa kukusanyika mbele zake Mwenyezi Mungu. Siku hiyo, siku iliyoitwa kila mwaka kuwa ni “siku ya upatanisho,” Israeli wote walihusika kiakili na kiroho kuzitupilia mbali dhambi zote maishani mwao. Hii ndiyo ahadi aliyotoa Mwenyezi Mungu kwa Israeli ya Kale katika siku ile ya aina yake.
Taurati Mambo ya Walawi 16:30 “Kwa maana siku hiyo upatanisho utafanywa kwa ajili yenu, ili kuwatakasa; nanyi mtatakaswa na dhambi zenu zote mbele za BWANA.”
Tukio hilo la kila mwaka lilihusiana na patakatifu pale pa mfano jangwani, pale pangekuwa kivuli cha tukio kubwa zaidi mwishoni mwa wakati. Tukio hilo la kale lilikuwa kivuli cha tukio ambalo tunaishi nalo sasa. Ni katika wakati huu ambapo Mwenyezi Mungu anapaswa kufanya jambo fulani la pekee. Anataka kuwatenga kabisa watu wake mbali na dhambi zao. Huko ni kutakaswa na dhambi ambako bado hatujawahi kukuona hapa duniani. Je, wewe na mimi tutakuwa na sehemu katika kutakaswa huko kunakofanyika mbinguni?
Amani tamu ya Mbinguni na iwe juu yako.
Aya zimenukuliwa kutoka DivineIslam’s Qur’an Viewer software v2.913
Kwa maelezo zaidi: www.salahallah.com
Isa atakuwa alama ya kukaribia kwa…
“Saa ya Hukumu!”
Sura 43:61
Az-Zukhruf
Sehemu ya Pili
Mfululizo na.36B