Assalamu’ alaikum!
Kurani Tukufu huelekeza kidole chake kwenye kundi lile liitwalo “Waliopewa Kitabu”. Msomaji anaombwa asome Sura 3:113-115. Aali Imran.
003:113 “Wao (Waliopewa Kitabu) si wote sawa. Katika (hao) Waliopewa Kitabu wamo watu waliotengenea – wanasoma Aya za Mwenyezi Mungu nyakati za usiku, na pia wanasujudu (yaani wamesilimu).”
003:114 “Wanamwamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, na wanaamrisha mema na wanakataza maovu na wanayaendea mbio mambo mema. Na hao ndio miongoni mwa hao watendao mema (kweli kweli).”
003:115 “Na heri yo yote watakayoifanya hawatakanushiwa (thawabu zake). Na Mwenyezi Mungu anawajua wanaomcha (wakajiepusha na makatazo yake na wakafanya maamrisho yake).”
Watu hao wanajulikana kama ‘Wakristo’. Hao wanaitwa ‘Waliopewa Kitabu’ (Maandiko ya Biblia). Lakini miongoni mwao limo kundi la pekee. Kurani Tukufu yasema kwamba ipo tofauti kati ya hao ‘Wakristo’ na ya kwamba ‘si wote sawa.’
Je, kundi hilo la pekee ni akina nani ambao Nabii Muhammad (jina lake na liheshimiwe) alivuta mawazo ya watu kuelekea kwao kwa namna ya ajabu kama hiyo, ya kuwa wao ni ‘miongoni mwa hao watendao mema kweli kweli’!
Hebu zingatia tabia zinazolitambulisha kundi hili la pekee kutoka katika Sura 3:113-115
1. si (Wakristo) wote sawa
2. katika (hao) waliopewa Kitabu wamo watu waliotengenea
3. wanasoma Aya za Mwenyezi Mungu
4. wanasujudu
5. wanamwamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho
6. wanaamrisha mema [wanafundisha kwa mamlaka yaliyo ya haki]
7. wanakataza maovu
8. wanayaendea mbio mambo mema [wanajitahidi kufanya yale yenye sifa njema]
9. hao ndio miongoni mwa hao watendao mema kweli kweli
10. na heri yo yote watakayoifanya hawatakanushiwa. [Mwenyezi Mungu anawajua]
Kurani Tukufu yasema hivi kuhusu kundi hilo la pekee, kwamba hao “ndio miongoni mwa hao watendao mema kweli kweli”. Iwapo hao ni miongoni mwa hao watendao mema kweli kweli, basi yale wayasadikiyo hayana budi kuwa ndiyo kweli yenyewe. Kama Mwenyezi Mungu anawaita kuwa wamo miongoni mwa hao watendao mema kweli kweli, basi, sisi hatuthubutu kabisa kuwakosoa. Lakini je! si afadhali sisi pia tungeweza kujifunza kitu kwao? Twaona ya kwamba watu hao wa pekee wanakishikilia kile ‘Kitabu’ (Maandiko ya Biblia) ambacho Nabii Muhammad kwa makusudi mazima alituelekeza sisi kwenye [Kitabu] hicho katika Kurani Tukufu (Al Maidah) Sura 5:46 … “Na tukawafundisha (Mitume hiyo) Isa bin Maryamu kuyahakikisha yaliyokuwa kabla yake katika Taurati, na tukampa Injili iliyomo ndani yake uongozi na nuru na isadikishayo yaliyokuwa kabla yake katika Taurati, na uongozi na mauidha kwa wamchao (Mwenyezi Mungu).”
Watu hao wanasadiki kwamba ni jukumu lao kujitoa kabisa kwa Mwenyezi Mungu pasipo kuzuia kitu, kuwa na utii kwake usio na swali. Watu hao wana maadili ya kiwango cha juu, ambayo yamejengwa juu ya Maandiko ya Biblia. Wanamheshimu Mwenyezi Mungu kuwa ndiye Mkuu kuliko wote, tena hawana mshirika ye yote (kama vile Maryamu au wale wengine waitwao watakatifu wanaoabudiwa) ambaye wanamfungamanisha na huyo Mungu kama Wakristo wengi sana wafanyavyo. Katika Injili maneno haya hunenwa: Yakobo 2:19 “Wewe waamini ya kuwa Mungu ni mmoja; watenda vema.” … na katika Marko (Isa al-Masih) Kristo Mwenyewe alisema… “Bwana Mungu wetu ni Bwana mmoja”. Watu hao hawazisujudu sanamu katika ibada yao kama wafanyavyo Wakristo wengi sana. Wanasadiki kwamba kuabudu sanamu au mifano iwayo yote kumekatazwa kabisa na Mwenyezi Mungu, kama ilivyoandikwa katika Taurati, Kutoka 20:4-5 “Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia. Usivisujudie wala kuvitumikia”. Watu hao wanajua kwamba kuabudu hiyo mifano na sanamu kumekatazwa kabisa katika Maandiko ya Biblia.
Yaendelea [Kurani Tukufu] kusema kwamba watu hao katika ibada yao kwa Mwenyezi Mungu ‘wanasujudu’, yaani, wanapiga magoti mbele zake Mwenyezi Mungu kama Daudi alivyoandika katika Zaburi (Taurati), Zaburi 95:6 “Njoni, tuabudu, tusujudu, tupige magoti mbele za BWANA aliyetuumba.”
Katika Sura 3:114 inatuambia sisi kwamba ‘wanakataza maovu’. ‘Hao’ miongoni mwa “wao Waliopewa Kitabu” wanakataza kula vyakula najisi (haramu) kama ‘Nyama ya nguruwe’. (Taurati) Mambo ya Walawi 11:7 “Na nguruwe, … yeye ni najisi kwenu.” Wanakataza matumizi ya vileo, tumbako, na vitu vingine vinavyodhuru (haramu) afya ya mwili ambavyo vinauangamiza. Wanaziheshimu Amri Kumi za Mwenyezi Mungu kama zilivyoandikwa katika (Taurati) Kutoka 20. Watu hao wanasadiki kwamba tunaishi katika “Siku za Mwisho” za historia ya dunia hii…
Waadventista Wasabato
Je! kundi hilo la pekee la “Waliopewa Kitabu” ambao juu yao Kurani Tukufu inaongea sifa nyingi sana ni akina nani? Lipo kundi la watu miongoni mwa “Waliopewa Kitabu” lijulikanalo kama: “Waadventista Wasabato (Seventh.Day Adventists)”. Hapa chini yapo maelezo mafupi kuhusu yale wanayoyaamini. Linganisha yale wayaaminiyo na kuelewa iwapo yanapatana na maelezo yaliyotolewa katika Sura 3:113-115? Je, hao ndilo lile kundi la “si wote” miongoni mwa waliopewa kitabu, yaani, ambao wamo miongoni mwa hao watendao mema kweli kweli?
Waadventista Wasabato wanaamini:
1. Kwamba wanamtumikia Mungu Mmoja [Allah] na kwamba hawamhesabii Mwenyezi Mungu kuwa anao washirika kama vile Bikira Maria na wengine waitwao watakatifu wanaoabudiwa. Injili Yakobo 2:19 ‘Wewe waamini kuwa Mungu ni mmoja; watenda vema..’…
2. Wanampa Mwenyezi Mungu roho zao zote. (Injili) Luka 10:27 ‘Akajibu akasema, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote; na jirani yako kama nafsi yako.’
3. Hawamtumikii Mwenyezi Mungu kwa njia ya sanamu na mifano, vitu hivyo vimekatazwa kabisa. Kutoka 20:4-6 “Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote …Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi, BWANA, Mungu wako [Allah], ni Mungu mwenye wivu…”
4. Wanaamini kwamba siku ya saba (siku ya mwisho) ya juma ni siku bora kuliko zote. Wanaiheshimu siku ile kwa kumfanyia ibada Muumbaji [Allah]. Ni siku ile iitwayo “Sabt” ambayo ina maana ya ‘pasipo kazi’ katika lugha ya Kiarabu. Wanazifuata amri zote za Mwenyezi Mungu kama zilivyotolewa katika (Taurati) Kutoka 20:8-11 ‘Ikumbuke siku ya Sabato uitakase. Siku sita fanya kazi, utende mambo yako yote; lakini siku ya saba ni Sabato ya BWANA, Mungu wako, siku hiyo usifanye kazi yo yote, wewe, wala mwana wako, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala mjakazi wako, wala mnyama wako wa kufuga, wala mgeni aliye ndani ya malango yako. Maana, kwa siku sita BWANA alifanya mbingu, na nchi, na bahari, na vyote vilivyomo, akastarehe siku ya saba; kwa hiyo BWANA akaibarikia siku ya Sabato akaitakasa.’ Wao wanaamini kwamba Mwenyezi Mungu ndiye Muumbaji na ya kwamba aliiumba dunia na vyote vilivyomo ndani yake kwa siku sita na kupumzika siku ya saba.
Sura 10:3
10:003 ‘Bila shaka Mola wenu ni Mwenyezi Mungu ambaye ameziumba mbingu na ardhi katika siku sita. Kisha akatawala juu ya Arshi yake [Kiti chake cha enzi]. Yeye ndiye anayepitisha mambo yote. Hakuna Muombezi ila baada ya idhini yake (Mungu). Huyu ndiye Mwenyezi Mungu, Mola wenu. Basi Muabuduni Yeye. Je! hamkumbuki (kuwa hayo mliyo nayo siyo mambo ya haki)? Sura 10:003 Yunus
Hebu fikiria tu jinsi wewe mwenyewe uwezavyo kuitumia siku nzima, yaani, siku ile ya mwisho, (ya saba) ya juma, siku bora kuliko zote, kwa ajili ya kujitoa kabisa kwake Mwenyezi Mungu! Kuitumia siku hiyo kumwabudu na kumsifu Mwenyezi Mungu, kushirikiana na kutiana moyo kila mmoja na mwenzake. Kuweka kando biashara yote na mambo ya ulimwengu huu, mambo yote yanayosambaratisha mawazo yako, na kuichukua familia yako kwenda kumwabudu Mwenyezi Mungu na kutumia muda huo pamoja na kila mmoja pengine kwa kutembea kimya kimya kuangalia viumbe vya asili. Kweli huu ndio mbaraka ambao wachache mno huutambua. Je, huo usingejumuisha kumpenda Mwenyezi Mungu kwa moyo wako wote?
Jambo la mwisho, watu hao ni wafuasi wa Isa al-Masih (Kristo aitwaye Masihi). Sura 3:055
3:055 (Kumbukeni) Mwenyezi Mungu aliposema: ‘Ewe Isa! Mimi nitakutimizia muda wako wa kuishi (hawatakuua hao maadui). Na nitakuleta kwangu, na nitakutakasa na wale waliokufuru, (hawataweza kukudhuru) na nitawaweka wale waliokufuata, juu ya wale waliokufuru, mpaka siku ya Kiyama. Kisha marejeo yenu yatakuwa kwangu, nikuhukumuni katika yale mliyokuwa mkihitilafiana.’ 3:055 Aali Imran. Msomaji anaombwa ajifunze juu ya Waadventista Wasabato.
BISMILA-HIR RAHMA-NIR RAHIM
Aya zimenukuliwa kutoka DivineIslam’s Qur’an Viewer software v2.913
Mafungu ya Biblia yanatoka katika Toleo la King James (KJV)
Kwa maelezo zaidi: www.salahallah.com
‘Waliopewa
Kitabu’
… si wote sawa!
Sura 3:113-115
Aali Imran
Mfululizo na. 02