Kiswahili 07. “Msiruke Mipaka kwa (kuvunja taadhima ya) Jumamosi [Sabato]”

BISMILA-HIR RAHMA-NIR RAHIM

 

Leo kuna somo jingine zuri sana la kujifunza. Je, Waislamu wanapaswa kuitunza siku ya Sabato “Sabt” kama siku ya kupumzika ambayo mtu hujizuia asifanye kazi yo yote?
Wengi katika dini ya Kiislamu huamini kwamba zile Amri Kumi zilizoandikwa kwa “kidole chake Mwenyezi Mungu” (Allah) hazina budi kutiiwa. Kile ambacho wengi wamepitiwa ni ukweli kwamba moja wapo ya hizi “Amri Kumi” imesahauliwa. Hata Wakristo wengi wanaodai kukifuata Kitabu hicho (Vitabu Vitakatifu vya Biblia) hawaijali moja ya hizo Amri kama zilivyoandikwa katika Taurati. Kusema kweli wengi wao wanaziangalia kwa chuki kubwa au kwa dharau kubwa Sheria hizo ambazo ni Takatifu kwa wanadamu.
Kwanza, twataka kujadili hoja hii, Je, Amri Kumi ni nini? Je, hivi yatupasa sisi kuishi kwa kuzifuata sheria hizi siku hizi? Twataka kuziangalia kwa makini hizo Amri Kumi kuona ni nini hasa. Zimeandikwa katika Taurati katika Kutoka 20 na Kumbukumbu la Torati 5 la (Vitabu Vitakatifu) na katika Injili yote ya Maandiko ya Biblia. Mkumbukeni Mstahiki Nabii Muhammad kile alichokifunua katika Kurani Tukufu kwamba Taurati iliyoteremshwa kwa Musa na Injili aliyopewa Isa al-Masih, vyote viwili vilikuwa kwa ajili ya mauidha kwetu. Hivyo kwetu ni uongozi, nuru, na kipimo cha hukumu. Angalia:
Sura 2:53 Al Baqarah
Sura 3:3 Aali Imran
Sura 21:48 Al-Aniva
Sura 10:94 Yunus
Sura 5:44 Al Maidah
Sura hizi ni baadhi tu ya kumbukumbu nyingi zilizomo ndani ya Kurani Tukufu kuhusu hivyoVitabu Vitakatifu vya Maandiko ya Biblia (Taurati na Injili).
Kielelezo cha Ibrahimu…
Watu wengi leo huona kwamba Ibrahimu yule wa zamani, alikuwa ni mtu aliyemheshimu Mwenyezi Mungu kwa moyo wake wote. Hivyo yeye amekuwa kielelezo fulani kwetu cha kufuata. Katika Vitabu vile Vitakatifu (Maandiko ya Biblia) twaambiwa yafuatayo kuhusu Ibrahimu na jinsi alivyoziona zile Amri Kumi za Mwenyezi Mungu. Katika Taurati, Mwanzo 26:5 “… Ibrahimu alisikia sauti yangu, akayahifadhi maagizo yangu, na amri zangu, na hukumu zangu, na sheria zangu.” Aya hii katika Taurati hutuambia sisi kwamba Amri Kumi za Mwenyezi Mungu zilifuatwa na Ibrahimu aliyeishi muda mrefu kabla ya siku za Musa. Hiyo pia inatuambia sisi ya kwamba watu wa nyakati zile za kale waliijua fika sheria ile ile ambayo pia ilirudiwa kwa Musa katika vilele vile virefu vya Mlima Sinai. Iwapo Ibrahimu anafikiriwa kuwa ni “Hanif” kati ya wale ambao kwa unyofu wa moyo wanamkaribia sana Mwenyezi Mungu, basi, sisi tungefanya vema kukifuata kielelezo chake Ibrahimu kwa kuzitunza pia Amri Kumi za Mwenyezi Mungu. Kufanya mambo yawe rahisi, hii maana yake ni kwamba Ibrahimu aliitunza Siku ya Saba ya juma kama siku ya ‘kupumzika’ kwa heshima yake Mwenyezi Mungu
.
“Kidole chake Mwenyezi Mungu”
Kisa cha Amri Kumi kimeandikwa katika Taurati (Kutoka 20). Wana wa Israeli waliokuwa wameokolewa kutoka utumwani Misri walipofika jangwani, Musa aliagizwa kwenda juu ya Mlima Sinai. Ni wakati ule alipokuwa kule alipopewa mbao mbili za mawe ambazo juu yake ziliandikwa zile Amri (Maneno) Kumi kwa kidole chake Mwenyezi Mungu. Kutoka 31:18 na Kumbukumbu la Torati 9:10.

004:154 “Na tukaunyanyua mlima juu yao (hao Mayahudi) kwa kufanya agano nao (la kufuata Taurati). Na tuliwaambia: ‘Liingieni lango (la nchi ya Shamu) hali ya kuinama (kama mnarukuu)”; (wakapinga). Na (pia) tukawaambia: “Msiruke mipaka kwa (kuvunja taadhima ya) Jumamosi [Sabato].’ ‘Na tukachukua kwao ahadi iliyo madhubuti’ …” Sura 004:154 (An-Nisaa [Wanawake]).

Je, Mwenyezi Mungu angemwita mtu Mnafiki kuwa ni Mtume wake?
Hili ni swali ambalo wengi wenu kwa hakika tayari mnalijua jibu lake. Hasha! Lakini basi, hatuna budi kujiuliza swali hili: Kama Nabii Mstahiki Muhammad angeweza kusema “Msiruke mipaka” katika suala la Sabato, je, si angeitwa kuwa ni ‘mnafiki’ endapo yeye mwenyewe asingeitunza hiyo Sabato? Kwa maneno mengine, Nabii huyu Mstahiki asingewataka watu kutii mojawapo ya Amri zake Mwenyezi Mungu wakati yeye mwenyewe haitii sheria iyo hiyo! Kwa ajili hii ushahidi upo wa kutosha kuwa huyo Nabii Mstahiki Muhammad ni lazima alikuwa ameitii pia ile Amri ya nne. Amri hii inatuambia sisi kupumzika Siku ya Saba ya juma kwa heshima yake Mwenyezi Mungu (Allah) na kutusaidia sisi kukumbuka kwamba Mwenyezi Mungu aliyeumba vitu vyote kwa siku sita. Katika maneno yaliyo dhahiri kabisa kutoka katika Kurani Tukufu imeandikwa kwamba Sabato isivunjwe, kwa kweli katika sura ifuatayo “laana” ilitamkwa na Mwenyezi Mungu juu ya wale waliokuwa “wavunjaji wa Sabato’.

004:047 “Enyi mliopewa Kitabu! Aminini tuliyoyateremsha yanayosadikisha yale yaliyo nanyi, kabla hatujazigeuza nyuso tukazipeleka kisogoni, au kabla ya kuwalaani kama tulivyowalaani watu (walioharibu utukufu) wa Jumamosi. Na amri ya Mwenyezi Mungu lazima kufanywa.” Sura 004:047 (An-Nisaa [Wanawake]).
Kielelezo cha Isa al-Masih…
Pengine kutoka kwa yule Mmoja aliyekuwa karibu sana na Mwenyezi Mungu twaweza kujifunza ukweli kuhusu Sabato na kama bado inafanya kazi yake hadi leo! Tunacho kielelezo chake Isa al-Masih aliyeteremshwa chini kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambaye alikuwa ndiye lile Neno kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ni kwa Isa al-Masih Injili ilitolewa. Katika Sura 3:45 twaambiwa kwamba Neno kutoka kwa Mwenyezi Mungu lilikuja kwa njia ya Isa al-Masih aliyepewa heshima. Kutoka kinywani mwa yule aliyeteremshwa chini tunayo kumbukumbu isemayo kwamba … Siku ya Sabato Isa alifundisha katika sinagogi. (Injili) Marko 1:21 “Wakashika njia mpaka Kapernaumu, na mara siku ya Sabato [Isa al-Masih] akaingia katika sinagogi, akafundisha.”
Lakini watu wengine wanataka kutoa hoja hii kwamba Sabato ilifanywa kwa ajili ya Wayahudi tu … lakini lile Neno kutoka kwa Mwenyezi Mungu lilisema haya yafuatayo: (Injili) Marko 2:27 “Akawaambia, Sabato ilifanyika kwa ajili ya mwanadamu, si mwanadamu kwa ajili ya Sabato.”
Wengine wangependa kupotosha au kunukuu vibaya fungu hili ili lisomeke ‘Myahudi’ badala ya kusomeka ‘mwanadamu’. Lakini hapo limeandikwa katika lugha inayoeleweka kwamba Isa al-Masih aliyeteremshwa chini kutoka kwa Mwenyezi Mungu na ambaye alikuwa miongoni mwa wale waliokuwa karibu sana na Mwenyezi Mungu, na kupewa heshima… (Sura 3:45), ametuambia kweli ya kwamba ‘Sabato ilifanyika kwa ajili ya mwanadamu’. Mwanadamu huyo anamaanisha binadamu wote. Lakini ni waumini wangapi wanaoutii ujumbe huu utokao kwa Mwenyezi Mungu? Je, watu hawaoni kuwa shughuli zao binafsi ni za maana kuliko shughuli yake Mwenyezi Mungu, katika hiyo Siku Yake Takatifu, ya Saba katika juma (Jumamosi), iitwayo ‘Sabt’ (Sabato)? Wengi wanavifanya hivyo Vitabu Vitakatifu kuwa kama ‘ubao wa kubashiria’(smorgasboard) ambao juu yake unachagua kile unachotaka. Ukichagua baadhi ya vitu na kuvikataa vingine. Je, hayo siyo yaliyokwisha kutokea katika ulimwengu wetu wa leo? Yuko wapi mtafutaji wa ile kweli aliye makini? Ni akina nani miongoni mwa watu ambao huyapa kipaumbele mambo ya Mwenyezi Mungu, na kutafuta kwa moyo wao wote kuyajua mapenzi yake? Katika Injili, Mathayo 4:4 inasomeka hivi … “Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu (Allah).” Kwa hiyo sisi hatujaachiwa [kazi ya] kuchambua na kuchagua wenyewe.
Je, Mwenyezi Mungu ni Kigeugeu?
Tunayo kumbukumbu isemayo kwamba juu ya vilele vya Mlima Sinai, Maneno ya Amri Kumi hayakuandikwa tu juu ya mawe kwa kidole chake Mwenyezi Mungu, bali pia maneno yale yalinenwa na Mwenyezi Mungu Mwenyewe! Taurati (Kumbukumbu la Torati 5:22 “Haya ndiyo maneno ambayo BWANA [Allah] aliwaambia mkutano wenu wote mlimani kwa sauti kuu toka kati ya moto, na wingu, na giza kuu; wala hakuongeza neno. Akayaandika juu ya mbao mbili za mawe, akanipa [mimi Musa].”
Tena akizitaja sheria zile zile … Kutoka 20:1 “Mungu [Allah] akanena maneno haya yote akasema” … Hivyo Mwenyezi Mungu (Allah) hakunena tu yale Maneno, bali p;ia aliyaandika Maneno yale ili sisi tusikosee. Hapa chini limenukuliwa Neno lililotoka kwake Mwenyezi Mungu.
Sheria ya Sabato kama ilivyoandikwa katika (Taurati) Kutoka 20:8-11 ‘Ikumbuke siku ya Sabato uitakase. Siku sita fanya kazi, utende mambo yako yote; lakini siku ya saba ni Sabato ya BWANA, Mungu wako, siku hiyo usifanye kazi yo yote, wewe, wala mwana wako, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala mjakazi wako, wala mnyama wako wa kufuga, wala mgeni aliye ndani ya malango yako. Maana, kwa siku sita BWANA alifanya mbingu, na nchi, na bahari, na vyote vilivyomo, akastarehe siku ya saba; kwa hiyo BWANA akaibarikia siku ya Sabato akaitakasa.’ Zingatia, Ee mpendwa msomaji , Mwenyezi Mungu aliibariki siku ile na kuitakasa.

Je, hivi Mwenyezi Mungu atazibadili au kuzigeuza Sheria zilizotoka mdomoni mwake? Kwa (swali) hilo sisi tunalijibu tu kwa Neno litokalo kwake Mwenyezi Mungu … Zaburi 89:34 “Mimi sitalihalifu agano langu, Sitalibadili Neno lililotoka midomoni mwangu.” Pia [soma] hapa: 1 Mambo ya Nyakati 17:27 “Nawe sasa umekuwa radhi kuibarikia nyumba ya mtumwa wako, ipate kudumu milele mbele zako; kwa maana wewe, BWANA, umebarikia, nayo imebarikiwa milele.” Basi, ni juu yetu kuchagua iwapo tunafuata na kutii kwa ukamilifu mapenzi yake au je, sisi twafanana na wasioamini wanaoyadharau Mapenzi yake Mwenyezi Mungu? Hebu na tuonekane miongoni mwa walio waaminifu, hili ndilo ombi letu kwako mpendwa msomaji. Kumbuka kwamba Mwislamu ni mtu anayelitii Neno lake Mwenyezi Mungu bila swali, je, hilo lisingeihusu [pia] Sabato?

Aya zimenukuliwa kutoka DivineIslam’s Qur’an Viewer software v2.913

Maandiko ya Biblia yanatoka katika Toleo la King James (KJV)

Kwa maelezo zaidi:
www.salahallah.com

“Msiruke
Mipaka kwa (kuvunja taadhima ya) Jumamosi
[Sabato]

Sura 4:154
An Nisaa

Mfululizo na. 07